Wakimbizi wa Burundi hawana matumaini
Wakimbizi
wa Burundi waliokimbilia nchini Rwanda kufuatia machafuko ya kisiasa
yanayoendelea nchini kwao wamepoteza matumaini ya kumalizika haraka
mgogoro wa nchi yao.
Raia hao
wa Burundi wapatao elfu 25 ambao wamekuwa wakiishi mjini Kigali huko
Rwanda tangu nchi yao ilipotumbukia katika lindi la machafuko, wamesema
kuwa, wamekosa matumaini ya kurejea makwao hivi karibuni na kwamba bado
wanasubiri utatuzi wa kadhia hiyo.
Kwa
mujibu wa wakimbizi hao, magogoro wa sasa nchini Burundi unashabihiana
sana na ule wa Rwanda kabla ya kutokea mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Wameongeza kuwa, kukosekana makubaliano baina ya serikali na wapinzani
ndiyo sababu kuu iliyowafanya kukosa matumaini ya kuweza kuhitimishwa
machafuko nchini Burundi. Wanyarwanda karibu milioni moja waliuawa
katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Kwa
mujibu wa Umoja wa Mataifa, hadi sasa machafuko nchini Burundi
yamesababisha mamia ya watu kuuawa na wengine zaidi ya laki mbili kuwa
wakimbizi. Wakimbizi elfu 75 kati yao wamekimbilia nchini Rwanda na elfu
25 miongoni mwao wanaishi mjini Kigali.(VICTOR)
Comments
Post a Comment