SBC yapunguza bei ya vinywaji vyake kutoka shillingi mia sita (600) hadi mia tano (500)
Dar es Salaam.
Kampuni ya SBC Tanzania
Limited, watengenezaji na wasambazaji wa vinywaji baridi imepunguza bei
ya vinywaji vyake kutoka shillingi mia sita (600) hadi mia tano (500)
kwa chupa yenye ujazo wa Mililita 350 na 300.
Hayo yamesemwa na Meneja
Mafunzo na Uwezeshaji Bw.Rashid Chenja alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa lengo la
kupunguza bei ni kutokana na hali ngumu ya uchumi iliyopo.
“Imekuwa vigumu kwa mnywaji
kuweza kudumu bei ya kinywaji akipendacho cha pepsi , gharama za maisha
zinapanda kila mwaka na soda imekuwa ghali kiasi cha wananchi wa kawaida
kushindwa kumudu kununua soda hivyo kampuni imeamua kupunguza bei”
alifafanua Meneja huyo.
Pia amesema kuwa kampuni ya SBC
Tanzania imefanya punguzo hilo kuanzia tarehe 16/11/2015 kwa vinywaji
vya Pepsi, Mirinda,7up, Mountain Dew na Evervess na maeneo yatakayo
husika na punguzo hilo la bei ni Dar es salaam,Morogoro, Dodoma, Pwani,
Tanga, Lindi, Mtwara na Zanzibar.
“Ni matumaini yetu mtaendelea
kutuunga mkono katika biashara yetu kwa kununua soda zetu kwa bei
iliyopendekezwa ya shilingi Mia Tano kwa chupa, shilingi elfu tisa mia
nne (9,400) kwa kreti moja na faida kwa wauzaji wa rejareja itakuwa ni
shilingi 2500 kwa kila kreti” aliongeza Bw. Chenja.
Mbali na hayo Kampuni ya SBC
Tanzania Limited inawashukuru wateja wake kwa kuwaunga mkono katika
biashara yao kwa kipindi cha miaka 14 hapa nchini.
Comments
Post a Comment