MBUNGE KINGU AELEZA SABABU YA KUKATAA POSHO ZA BUNGE
Elibariki Kingu akitoa ufafanuzi wa jambo mara baada ya kuulizwa maswali kutoka kwa wanahabari.
Kutoka kushoto ni Hamisi Ngila, aliyekuwa mpinzani wa Kingu katika kura za maoni ndani ya CCM, Elibariki Kingu na Gerard Lukas.
Elibariki akisoma taarifa yake aliyokuwa ameiandaa kwa wanahabari.
Wanahabari wakichukua tukio.
MBUNGE wa
Singida Magharibi kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Elibariki
Kingu amesema sababu za kuandika barua kwa Katibu wa Bunge kusimamisha
posho zake zote za vikao ’sitting allowance’ ni kutaka fedha hizo
kupelekwa kwenye mfuko wa jimbo lake kwa ajili ya shughuli mbalimbali za
kimaendeleo.(P.T)
Akizungumza
na wanahabari leo katika hoteli ya Travertine jijini Dar es Salaam,
Kingu amesema dhamana aliyopewa si kwa vile yeye ni bora kuliko
aliochuana nao, bali ni matumaini makubwa ya wapigakura wake kwake.
Alisema
wapiga kura wake wana kero kama huduma za maji, afya, ujenzi wa vyumba
vya madarasa na uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano.
Ni kwa ajili hiyo, alisema anajiona ana dhamana na deni la kuhakikisha utekelezaji wa utatuzi wa kero hizo jimboni kwake.
Amefafanua
kuwa ili aweze kuikemea serikali katika matumizi yasiyo ya lazima, ni
vyema yeye kama Mbunge akatae kuchukua malipo ya vikao vya bunge kwa
kipindi chake chote cha miaka mitano.
Alisema
licha ya kutambua kuwa fedha hizo zipo kikanuni, alisema zitatolewa
kupitia akaunti maalum ya mfuko wa jimbo lake utakaokuwa na usimamizi wa
watu saba, aliowataja kuwa ni Mkuu wa Wilaya, Shekhe wa Wilaya ya
Ikungi, Mchungaji wa Kanisa la SDA, Mchungaji wa kanisa la CCT,
Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste, Padre mmoja kutoka Kanisa Katoliki na
Afisa mipango wa wilaya.
Tayari
katika siku chache ambazo amekaa bungeni kuapishwa, amesema posho yake
imenunua mifuko 100 ya saruji, ikiwa ni hatua ya kwanza ya utekelezaji
wake wa ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mpetu kata ya Muhintiri.
Alisema
kitendo chake cha kutochukua posho hizo ni changamoto kwa wabunge
wenzake, akisema hawana sababu ya kuchukua posho ya vikao kwa vile ni
kazi yao wanayolipwa mishahara.
“Ninaomba
niwape mchanganuo mdogo, kama jambo hili la kukataa posho za vikao
litatekelezwa ipasavyo na kupelekwa katika huduma muhimu za kijamii,
kuna wabunge 394 na vikao kisheria ni siku 182, wabunge tunalipwa
shilingi 220,000 kushiriki kikao cha siku moja.
“Fedha
hizi kama zitaondolewa au wabunge wenzangu wataridhia kutokuchukua, basi
tutakuwa tumeokoa zaidi ya shilingi bilioni kumi na tano milioni mia
saba sabini na tano kwa muda wa mwaka mmoja,” amesema Kingu.
Kuhusu
hotuba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, Kingu amesema anaunga mkono kwa
kufuta safari za nje kwani hatua hiyo italeta nidhamu ya uwajibikaji
katika maeneo mbalimbali ya kazi na kuwapata wafanya kazi halisi
watakaoweza kuifikisha Tanzania katika kuwa nchi ya asali na maziwa.
Comments
Post a Comment