KIPINDUPINDU CHAPUNGUA DAR
Idadi ya
wagonjwa wa kipindupindu jijini Dar es salaam imepungua kufikia wagonjwa
kumi na mbili (12) kwa mkoa mzima, huku wilaya ya Temeke ikiwa na
wagonjwa saba,Kinondoni wagonjwa wanne na Ilala ikiwa na mgonjwa mmoja
Haya
yamezungumzwa na Mratibu wa Magonjwa ya kuambukiza wa Jiji la Dar es
salaam Bw. Alex Mkamba ofisini kwake leo akielezea jinsi gani mkoa
umefanikisha kupambana na kipindupindu kwa kuzingatia usafi katika jiji.
Ameongeza
kuwa katika kufanikisha mapambano dhidi ya kipundupindu wametoa mafunzo
juu ya mbinu shirikishi ya namna ya kujikinga na kipindupindu kwa
watendaji wa mitaa na pia imewahimiza kukagua maeneo yao na kuwapa
kibali cha kufunga maeneo ya biashara au maeneo yatoayo huduma za
chakula yasiyozingatia usafi.
Akielezea
kuhusu huduma kwa wagonjwa wa kipindupindu jijini Dar es salaam mratibu
huyo amesema jiji lina dawa za kutosha za kuhudumia wagojwa ipasavyo
kwa kuwapatia huduma bora zaidi kuendana na kasi ya maambukizi yaliyopo.
“ hata
leo Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa dawa za kusafishia maji (Water
Guard) maboksi 45 kwa kila wilaya” Mkamba alifafanua.
Aidha
alisema serikali imejipanga katika kudhibiti maambukizi mapya kwa
kuwapima wagonjwa kabla na baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini na
aliwashauri wananchi kubadili tabia kwa kuhakikisha usafi unafanyika pia
kuchemsha maji na kuufanya usafi kuwa ni tabia yao ya kila siku.
Mpaka sasa jumla ya watu 55 wamefariki dunia kwa ugonjwa wa kipindupindu jijini Dar es salaam.(P.T)
Comments
Post a Comment